Jumapili, 11 Agosti 2013

Wanaopelekwa ualimu wawe wa alama za juu

Happiness Mnale

KWA muda mrefu vyuo vya ualimu nchini vimekuwa vikidahili wanafunzi wenye alama za chini kusomea ualimu, ikiwa ni mojawapo ya mikakati ya serikali kukabiliana na uhaba wa walimu shuleni.
Mtu asiyeona kumwelekeza njia mwingine kama yeye ni jambo lisilowezekana. Hakutakuwa na kitu kitakachotoka, zaidi ya kuendeleza ujinga.
Leo tumeshuhudia matokeo ya mtihani wa ualimu uliofanyika Mei mwaka huu yaliyotangazwa na Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) yakionesha kuwa wahitimu wa ngazi ya stashahada 2,906 wanatakiwa kurudia mitihani.
Matokeo hayo yanaonesha namna kiwango cha elimu kinavyozidi kuanguka na kuliacha taifa katika giza totoro.
Si siri kwamba taaluma ya ualimu imeanguka sana ikilinganishwa na awali, enzi ya uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Mwalimu aliyefeli hawezi kujiamini anapofundisha na aghalabu hawezi kukidhi mahitaji ya wanafunzi, hasa wale wenye uwezo mkubwa wa kuhoji mambo, ambao mara nyingi huitwa wasumbufu na walimu wasiojimudu.
Walianza wanafunzi wa darasa la saba kufeli, wakafuata kidato cha nne na sita na sasa ni walimu watarajiwa ambao tuliamini wao ndio nguzo ya kutuokoa katika anguko la elimu nchini.
Ubora wa elimu umeendelea kushuka siku hadi siku hata kuonekana kawaida kwa wanafunzi wanaomaliza darasa la saba kutojua kusoma wala kuandika.
Isitoshe uduni wa elimu kwa sasa unaendelea kushamiri ngazi zote, yaani kuanzia shule za msingi, sekondari, vyuo vya kawaida na hadi vyuo vikuu, ambapo wanafunzi wanamaliza na kutunukiwa vyeti wakiwa na maarifa finyu na uwezo mdogo wa kufikiri.
Siasa ya nchi hii na porojo zisizotekelezwa zimetufikisha hapa tulipo, badala ya viongozi kutafuta njia ya kulikomboa taifa katika giza la elimu nchini, wao wanaendelea kutangaza kiwango cha elimu kinapanda kila uchao, huku matokeo ya mitihani yakiwaumbua.
Siri ya kufeli kwa wanafunzi katika kila ngazi ya elimu ni kutokana na serikali kutotimiza madai ya walimu katika ngazi husika, kilio cha walimu hao hakifanyiwi kazi kwa uzito unaostahili.
Walimu wanapotaka haki yao baada ya serikali kutimiza na kukaa meza moja ya mazungumzo ili kupata mwafaka, wamekuwa wakifikishwa mahakamani na kurejeshwa kazini kwa amri, madhara ya jambo hilo ni kinyongo kinachofanya kuwapo mgomo wa kisiri.
Nashawishika kuamini kuwa matokeo mabaya ya mitihani kwa mwaka huu yanaonesha dhahiri kuwa walimu hawatimizi wajibu wao ipasavyo. Sauti ya Jumapili inapendekeza kuwa ni vema nafasi ya ualimu wakachaguliwa wanafunzi waliofanya vizuri, ikiwamo kutimiza mahitaji ya walimu na kuhakikisha masilahi ya sekta hii muhimu yanapewa kipaumbele.
Ni vema serikali ikakubali kukaa meza moja na walimu, maana ukiangalia kwa makini utagundua kuwa ni kweli mgomo wa kisirisiri upo na ndiyo sababu kubwa ya anguko la elimu.
Mwalimu mmoja alinieleza kuwa siku zote binadamu huvumilia maumivu kwa muda mrefu lakini siku atakayochoka atapiga kelele na kutaka kusaidiwa.
Kauli hii inaniambia kuwa walimu wameteseka vya kutosha, sasa kelele zao zinaonesha kwa vitendo, ambavyo ni kutotimiza wajibu wao ipasavyo, hali inayosababisha elimu kuanguka.
Kikubwa katika kuinua elimu kwa nchi ni kuweka mikakati na matarajio ya elimu bora ndani ya jamii yanayotokana na mafunzo bora ya walimu, ikiwamo kuhakikisha wanawekewa mazingira bora ya kufanyia kazi yao.
Pia ni vema tukaweka kando siasa za maji taka katika masuala ya msingi yanayolikumba taifa, ili wataalamu wa mambo ya ualimu watuzalishie walimu wenye tija watakaokomboa taifa kutokana na anguko la elimu.
Serikali ikitimiza mahitaji ya walimu naamini elimu ya nchi hii itanyanyuka, ikiwamo kuwapo sababu ya kuwabana ili kutimiza wajibu wao, maana wanachokidai watakuwa wamekamilishiwa.
Vilevile hakuna haja ya kuunda tume kila uchao wakati sababu ya anguko la elimu inafahamika, fedha za uundwaji wa tume hizo ni vema zikaingizwa katika mkakati wa kuinua elimu nchini.
Habari hii ni kwa hisani ya gazeti la mtanzania daima

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni