Jumamosi, 17 Agosti 2013
AZIMIO LA KAZI
AZIMIO LA KAZI
Ni mpangilio au utaratibu unaomwezesha mwalimu kuchanganua muhtasari wa somo na kupanga mada na jinsi atakavyozifundisha katika kipindi cha wiki , mwezi, na muhula.Ni mpango wa ufundishaji kwa kipindi fulani.
Umuhimu wa azimio la kazi
Humsaidia mwalimu kwenda na mtiririko mzuri wa mada.
Humwonyesha mwalimu muda wa kufundisha kila mada.
Huonyesha zana/vifaa/njia ya kumsaidia mwalimu katika ufundishaji wake.
Kuonyesha malengo ya ufundishaji wa somo hilo katika muda aliopanga.
Wakati wa kuandaa andalio la somo kuna mambo ambayo yanatakiwa kuzingatiwa,
Kuangalia kalenda au ratiba ya shule ambayo itakuongoza katika kuandaa azimio lako la kazi kwa kigezo cha muda.
Kusoma kwa makini muhtasari wa somo la kiswahili na kuweza kubaini mada, malengo , zana, na ujuzi ambao utatakiwa wanafunzi wako waupate katika mada husika.
Kuhakikisha kwamba vifaa vya muhtasari, vipo na vinatosheleza mfano, vitabu vya kiada, vitabu vya ziada, kiongozi cha mwalimu, kitabu cha mwalimu, na kitabu cha mwanafunzi.
VIPENGELE VYA AZIMIO LA KAZI
Ujuzi ni uwezo wa kufikiri, na kutenda anaoyarajiwa aujenge mwanafunzi kwa kupitia mada/maudhui kwa ushirikiano wa mwalimu na mwanafunzi, mwanafunzi na mwalimu, mwanafunzi na mazingira yake.
Katika kusoma ujuzi uliopo katika muhtasari wa somo la kiswahili , inakupasa kujua ujuzi ni upi, na maudhui ni yapi, kwani ujuzi huohuo huweza kujengwa na maudhui mengine.
Ujuzi hujengwa kwa vitendo vinavyojitokeza katika malengo mahsusi. Vitendo vya malengo mahsusi ndivyo vinavyoleta matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji ambao ni ujuzi.
Malengo mahsusi lengo ni lazima libebe kitendo kitakachowezesha ujuzi kutokea. Mada ndogo inaweza ikawa na malengo mengi yakibeba vitendo mbalimbali vitakavyotumika kujenga ujuzi.
Katika kuunda malengo ni vizuri ukazingatia vitendo vya kiwango cha juu vya kufikiri na kutenda kama , kueleza,kuchambua, kuunda,kuchanganua, kutofautisha, kutathmini, kubuni , kubainisha,kuhusianisha n.k. Viwango vya chini vya kufikiri na kutenda ni kutaja,kuorothesha,kuonyesha n.k kwa hiyo kazi ya mwalimu ni kumsaidia mwanafunzi kuinua kiwango chake cha kuunda vigezo vya kufikiri na kutenda.
Sifa za malengo mahsusi : – Ni lazima libebe kitendo kinachopimika wakati unapofundisha.
– Malengo yahusiane na kiwango cha uwezo wa mwanafunzi.
– Muda wa malengo utajwe waziwazi
– Kiwango cha kufikia kila lengo kiwezeshwe.
– Kipindi kimoja kisiwe na malengo mengi.
Mwezi na Wiki Katika kugawa muda unatakiwa kuzingatia idadi ya vitendo vitakavyofanyika ili mwanafunzi ajenge ujuzi. Kuna baadhi ya vitendo vinahitaji muda mrefu na vingine vinahitaji muda mfupi kukamilika.
Vipindi Idadi ya vipindi itazingatia na uzito na wigi wa vitendo katika mada husika. Jiulize vitendo vya kiwango cha juu vina uzito sawa na vitendo vya kuchunguza? Katika muhtasari umepewa muda wa idadi ya ya jumla ya vipindi kwa mada kuu, hakikisha kuwa umevigawa kwa uwiano sawa kulingana na vitendo.
Vitendo vya Ufundishaji Kumbuka unapoandika vitendo vya ujifunzaji wewe ni mwezeshaji/wewe ni msaada kwa mwanafunzi wako katika utendaji wake. Katika kuandika vitendo nya ufundishaji unatakiwa kuonyesha yale matendo yote utakayoyafanya mwalimu pamoja na mifano katika uwezeshaji wako.
Vitendo vya ujifunzaji Unapoandika vitendo vya ujifunzaji unatakiwa uvichukue ndivyo vitendo vya msingi vitakavyoleta kujengwa ujuzi. Lugha itakayotumika ionyeshe kuwa mtendaji mkuu ni mwanafunzi. Mfano Wanafunzi, kuchora, kueleza,Kujibu maswali ya mwalimu, kujadiliana,kutafsiri,kueleza, kusoma, kujadili, kufupisha n.k
Vifaa/zana Matumizi ya zana katika kujifunzia na kufundishia ni nyenzo muhimu sana kwa sababu inatumika katika ujenzi wa maana kwa kile mwanafunzi atakachojifunza. Vilevile zana humsaidia mwalimu katika kumrahisishia kazi yake ya kufundisha.
Rejea, Mwalimu atapaswa kuonesha vitabu vya rejea katika mada atakayoifundisha, Kumbuka rejea siyo vitabu tu, bali inahusisha vitu vingine kama majarida, magazeti,vipeperushi, vipindi vya redio, kanda za video, chati na makala mbalimbali na intaneti.
Upimaji, katika upimaji tunaangalia ufanisi wa ujifunzaji na ufundishaji uliofanyika katika malengo mahsusi. Upimaji huu unahusu vitendo hivyo vimefanyika kwa kiasi gani kuleta ujuzi. Mfano, mwalimu anaangalia ni jinsi gani vitendo vya ufundishaji na ujifunzaji vimefanikiwa.
Maoni, Inahusu hatua au ushauri utakaouchukua baada ya kufanya upimaji.
Mfano wa muundo wa azimio la kazi
Jina la mwalimu :………………. Mwaka:………………………..
Shule: …………….. Muhula:…………………………
Somo: ……………… Darasa:……………………………..
Ujuzi
Malengo
mwezi
wiki
Mada kuu
Mada ndogo
vipindi
v/ufundishaji
v/ufundishaji
vifaa/zana
rejea
Upimaji
maoni
Jisajili kwenye:
Chapisha Maoni (Atom)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni