Na Felix Mwakiyembe
CHANGAMOTO kubwa inayoikabili sekta ya elimu nchini ni ubora wa elimu, na hata Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inalitambua hilo ambapo moja ya malengo yake katika kipindi cha miaka 50 ijayo ni kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote.
Ni changamoto ambayo imetokana zaidi na upanuzi mkubwa uliofanyika kwenye sekta hiyo katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru, kuanzia ngazi ya elimu ya awali hadi ile ya chuo kikuu, elimu ya watu wazima pamoja na ile ya ufundi.
Kutokana na changamoto hiyo, wananchi walio wengi kuanzia wale wa kawaida hadi wana taaluma na hata baadhi ya viongozi wamekuwa wakiamini kwamba hakuna maendeleo yaliyofikiwa kwenye sekta ya elimu tangu kupatikana kwa uhuru wa Tanzania Bara miaka 50 iliyopita.
Takwimu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinatoa jibu la mkanganyiko huo kwa kuonyesha hali ya elimu nchini ilivyokuwa kabla ya uhuru na ile baada ya uhuru, na ni kwa kufanya ulinganisho wa nyakati hizo mbili ndipo tunaweza kufikia hitimisho la hoja kuhusu maendeleo ya sekta ya elimu nchini.
Elimu kabla ya uhuru
Nyaraka mbali mbali zilizopo zinabainisha kwamba mfumo wa elimu uliokuwepo kabla ya uhuru ulikuwa ni wa kibaguzi, elimu ilitolewa kwa kuzingatia matabaka ya rangi, ambapo Mwafrika alikuwa ni daraja la mwisho kabisa katika ubora, daraja la tatu, Muasia akawa daraja la pili na Mzungu alikuwa ndiye wa daraja la juu kabisa, la kwanza.
Matabaka haya yalionekana wazi wazi kwenye mpangilio wa shule, mathalani, mwaka 1960, kulikuwa na shule za msingi 3,270 zilizokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 450,626 lakini zikiwa zimegawanywa kwa kuzingatia rangi ambapo za Waafrika zilikuwa 3,115 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 431,056, na wasio Waafrika zilikuwa 155 zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 19,570.
Mfumo huo wa kitabaka katika utoaji elimu ulikuwepo hata kwenye shule za sekondari ambako nako ilitolewa kwa misingi ya matabaka ya rangi.
Hata hivyo takwimu zilizotolewa na Wizara ya Elimu zinaonyesha kwamba kwa elimu ya sekondari ya juu, Waasia na Wazungu hawakusomesha watoto wao hapa nchini bali waliwapeleka kusoma nje.
Mfumo wa elimu kabla ya uhuru uliweka shule ya msingi kuwa ya miaka minne tu, ambayo ni darasa la kwanza hadi la nne. Hata hivyo, kuwepo kwa ada ilikuwa kikwazo kwa wazazi wengi kusomesha watoto, ada ilisababisha nafasi katika shule za msingi na sekondari kutojazwa kutokana na Waafrika wengi kutozimudu.
Elimu ya ufundi stadi waliyopatiwa Waafrika ilikuwa katika daraja la chini kama vile uhunzi, mafundi bomba, fundi seremala, fundi mchundo, rangi, viatu na ushonaji, na mafunzo haya yalitolewa katika shule za Ufundi Ifunda iliyokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 249 na Shule ya Ufundi Moshi iliyokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 390.
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa anabainisha kuwepo kwa matabaka kwenye mfumo wa elimu kabla ya uhuru wakati akitoa taarifa ya sekta ya elimu nchini wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya uhuru kwenye viwanja vya Mnazi Mmoja, Dar es Salaam hivi karibuni.
Waziri Kawambwa anaongezea akisema kuwa elimu iliyotolewa kabla ya uhuru haikutoa kipaumbele kwa masomo ya sayansi ambayo ni mama wa uvumbuzi, na kwamba hapakuwepo na chuo kikuu hata kimoja hadi miezi saba kabla ya uhuru kilipoanzishwa chuo kikuu kishiriki chini ya Chuo Kikuu cha London.
Elimu baada ya uhuru
Mara baada ya uhuru yalifanyika mabadiliko makubwa katika mfumo mzima wa elimu nchini ikiwemo kufuta utoaji elimu kwa kuzingatia matabaka ya rangi.
“Mfumo wa utoaji elimu ulifanyiwa marekebisho ili kupata mfumo unaofaa kurudisha heshima na utamaduni wa Mtanzania na kukidhi mahitaji ya jamii na nchi huru,” anasema Waziri Kawambwa na kuongeza:
“Serikali ilitoa elimu kwa watoto wote bila ubaguzi, muda wa elimu ya msingi uliongezwa kutoka miaka minne hadi nane mwaka 1965 muda wa kusoma Elimu ya Msingi ulipunguzwa na kuwa miaka saba kwa sababu za kifedha.”
Kwa mujibu wa Waziri Kawambwa ufutaji wa darasa la nane ulifanyika kwa awamu tatu, ya kwanza ikiwa mwaka 1965 ambapo ilihusisha mikoa ya Arusha, Pwani, Kilimanjaro, Morogoro na Tanga, awamu ya piIi ilikuwa mwaka 1966 kwa mikoa ya Kigoma, Mara, Tabora, Shinyanga, Ziwa Magharibi na Mwanza na awamu ya tatu ilifanyika mwaka 1967 ikihusu mikoa ya Mtwara, Ruvuma, Mbeya Iringa, Dodoma na Singida.
Lugha ya kufundishia ni miongoni mwa zana muhimu sana katika mchakato mzima wa utoaji elimu, na ni kwa kuzingatia ukweli huo, serikali iliamua lugha za Kiswahili na Kiingereza kuwa lugha rasmi za kufundishia shule za msingi kuanzia mwaka 1964.
Historia ya maendeleo ya sekta ya elimu nchini inaonyesha kwamba, mwaka 1968, Serikali ilienda mbali zaidi kwa kukifanya Kiswahili kuwa lugha rasmi ya kufundishia katika shule za msingi.
Hatua hii ya serikali ni wazi ilizingatia zaidi kanuni zinazotumika kuteua lugha rasmi ya kufundishia, kwamba iwe ni ile inayofahamika na wanafunzi, na kwa Tanzania haikuwa nyingine zaidi ya Kiswahili.
“Kuwasaidia wanafunzi wa shule za msingi kufuata na kuelewa vizuri masomo yao na pia kukuza, kuendeleza na kurithisha utamaduni na Lugha ya Taifa,” anasema Waziri Kawambwa akizungumzia msingi wa uamuzi huo wa serikali.
Hata hivyo, hatua hiyo haikufuta kabisa Kiingereza mashuleni, lugha hiyo ilitumika katika shule za sekondari na vyuo na kwa shule za msingi kilibaki kama somo kwa baadhi ya madarasa.
Maeneo mengine yaliyofanyiwa marekebisho mara baada ya uhuru ni pamoja na kuandaliwa kwa muhtasari wa aina moja kwa nchi nzima ukitilia mkazo kazi za mikono na mambo muhimu ya kukuza umoja na maendeleo ya haraka kwa taifa.
Mwaka 1972, yalifanyika mabadiliko katika mitaala ili kukidhi mahitaji ya taifa, ambapo kutokana na mabadiliko hayo ilianzishwa elimu ya michepuo ya kilimo, ufundi, biashara na sayansi kimu katika elimu ya sekondari ili kutoa stadi za mwelekeo wa kazi, kuoanisha nadharia na vitendo, kuhimiza shule kuzalisha mali kwa madhumuni ya kusaidia kupunguza gharama ya elimu kwa serikali.
Pamoja na michepuo hiyo, ulianzishwa pia mchepuo wa Jeshi la Ulinzi katika shule za sekondari za wavulana na wasichana za Tabora mwaka huo huo wa 1972.
Mwaka 1975 serikali ilifanya maamuzi mengine mazito katika sekta ya elimu kwa kuanzisha Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Wote uliojulika zaidi kama UPE ikiwa ni kifupisho cha mpango huo kwa kiingereza, Universal Primary Eduction, hatua ambayo ilisababisha kupanuliwa kwa programu za mafunzo ya ualimu.
Kuanzishwa kwa mpango wa kuwachagua wanafunzi kwa kutumia kota za mikoa ili kusaidia kuwapa nafasi sawa watoto kutoka katika maeneo ya nchi yaliyokuwa na maendeleo hafifu kielimu.
Utaratibu mpya wa uteuzi wa wanafunzi kuingia sekondari ulianzishwa ambapo ziliundwa kamati za mikoa za uchaguzi wa kuingia sekondari lengo likiwa kusimamia haki na kutoa nafasi sawa za kuingia sekondari kwa watoto kutoka sehemu zote za nchi.
Mitihani ya Kidato cha pili kufutwa ili vijana wengi zaidi waweze kupata elimu ya sekondari kwa miaka minne badala ya miwili, hivyo kuliwezesha taifa kujipatia wataalamu wake.
Mwaka 1975, serikali ilisitisha mitihani ya kutoka nje ya nchi na kuanzisha Mitihani ya Taifa katika mfumo rasmi wa shule, ili kuokoa fedha za kigeni na kuliwezesha taifa kutathmini mitaala yake kwa misingi ya falsafa ya Elimu ya Kujitegemea.
Karo kwa shule za sekondari za Serikali ilifutwa ili kuwapa fursa watoto wenye sifa lakini waliotoka katika familia zenye vipato duni kuweza kujiunga katika shule za sekondari. Hali hii iliongeza idadi ya wanafunzi waliojiunga na shule za serikali.
Mwaka 1961, Serikali za Mitaa zilipewa jukumu la kusimamia shule za msingi na kuundwa Mamlaka za Elimu za Serikali za Mitaa zilizopewa madaraka ya kuendesha na kusimamia Elimu ya Msingi.
Katika mfumo huo mpya, serikali za mitaa zilichangia asilimia 40 ya gharama za elimu na serikali kuu asilimia 60 iliyobaki. Matokeo ya hatua hiyo ni ongezeko kubwa la uandikishaji wa wanafunzi kutoka 486,470 mwaka 1961 hadi 753,114 mwaka 1967.
Mfumo mpya wa elimu ulizingatia vile vile elimu ya juu kwa kuanzishwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1970, kikiwa cha kwanza hapa nchini, na pia kuweka umuhimu katika elimu ya watu wazima.
Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu ya Watu iliyoanzishwa mwaka 1961 na Chuo cha Kivukoni kilichoanzishwa mwaka 1963 ndio waliokabidhiwa jukumu la kutoa elimu hiyo wakati huo.
Mafanikio miaka 50 ya uhuru;
Mafanikio katika sekta ya elimu yanajibainisha katika maeneo yote nchini, yakiwemo ya kijamii, kisiasa na kiuchumi ambako sekta hiyo imeweza kuzalisha wataalamu takribani kwenye kila eneo, kama vile watalaamu wa afya, elimu, maji, wahandisi, nishati, madini, hali ya hewa, kilimo, usafiri, sayansi na teknolojia na wengine wengi.
Takwimu kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi zinaonyesha kuwepo kwa mafanikio makubwa kwenye sekta hiyo katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru, ikiwemo ongezeko la shule za msingi kutoka 3,270 mwaka 1961 hadi 16,001 mwaka 2011 (za Serikali 15,412 na za Binafsi 589), huku uandikishaji ukiongezeka kutoka wanafunzi 486,470 mwaka 1961 hadi 8, 363,386 mwaka 2011.
Mafanikio mengine yanatajwa kuwa ni pamoja na ongezeko la walimu kutoka 9,885 mwaka 1961 hadi 175,449 mwaka 2011 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 1,619.2, huduma za uendeshaji na usimamizi wa shule za awali, asingi, na sekondari zimekuwa karibu zaidi na walengwa kwa sababu ya zoezi la ugatuaji ambalo limeimarisha umiliki wa shule kwa jamii.
Shule za Elimu Maalumu zimeongezeka kutoka nne za wamisionari (Tabora, Buigiri, Irente na Uhuru Mchanganyiko) mwaka 1961 hadi kufikia 251 mwaka 2011. Aidha, kuna Elimu Jumuishi katika shule zote za msingi. Idadi ya wanafunzi wenye ulemavu imeongezeka kutoka wanafunzi 1,000 mwaka 1960 hadi kufikia 30,433 mwaka 2011.
Shule za sekondari zimeongezeka kutoka 41 (zikiwemo za binafsi mbili) mwaka 1961, hadi 4,367 mwaka 2011 (za Serikali 3,425 na za binafsi 942), huku uandikishaji wa wanafunzi katika shule ukiongezeka kutoka wanafunzi 11,832 mwaka 1961 hadi 1,789,547 mwaka 2011, sawa na ongezeko la asilimia 1,5024.6.
Walimu wa shule za sekondari nao wameongezeka kutoka 764 mwaka 1961 hadi 52,146 mwaka 2011, na uandikishaji wa kidato cha kwanza katika shule za Serikali umeongezeka kutoka wanafunzi 4,196 mwaka 1961 hadi 403,873 mwaka 2011, wakati uandikishaji katika kidato cha tano pia umeongezeka kutoka wanafunzi 236 mwaka 1961 hadi 30,265 mwaka 2011.
Vyuo vya Ualimu vimeongezeka kutoka vitatu, vyote vikiwa vya serikali, mwaka 1961 hadi vyuo 103 mwaka 2011 (vya Serikali 34 na binafsi 69).
Uandikishaji umeongezeka kutoka wanachuo 1,723 mwaka 1961 hadi 37,698 mwaka 2011, na idadi ya wakufunzi imeongezeka kutoka 164 mwaka 1961 hadi 1,833 mwaka 2011.
Vyuo vya Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi vimeongezeka kutoka vitatu mwaka 1961 hadi kufikia 912 mwaka 2011 na uandikishaji wa wanafunzi katika vyuo hivyo umeongezeka kutoka wanafunzi 1872 mwaka 1961 hadi kufikia 187,257 mwaka 2011.
Kwa upande wa elimu ya juu, vyuo vikuu vimeongezeka kutoka Chuo Kikuu kishiriki kimoja mwaka 1961 hadi vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki 40 (vya Serikali ni 11 na vya Binafsi 29) mwaka 2011, ambapo uandikishaji umeongezeka kutoka wanafunzi 14 mwaka 1961 hadi 104,130 mwaka 2011.
Idadi ya wanafunzi waliopata elimu ya msingi kupitia Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Watoto Walioikosa (MEMKWA) iliongezeka kutoka 1,500 mwaka 2001 hadi 185,206 mwaka 2007 na kushuka hadi 82,458 mwaka 2011.
Wanafunzi kupitia mpango huo wa MEMKWA waliofaulu na kujiunga na shule za sekondari iliongezeka kutoka 63 mwaka 2001 hadi 2,363 mwaka 2007 na 2,776 mwaka 2011.
Watu Wazima waliojiandikisha katika madarasa ya Elimu ya watu wazima nayo iliongezeka kutoka 600,000 mwaka 1961 hadi 2,059,359 mwaka 1975, lakini hata hivyo mwaka 2011 ilipungua kufikia 1,050,517.
Hayo ni machache tu katika mafanikio mengi yaliyorodheshwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi yaliyopatikana tangu uhuru.
Mbali ya ubora, zipo changamoto kadhaa zinazoikabili sekta ya elimu nchini ikiwemo kuinua kiwango halisi cha uandikishaji (Net Enrolment Ratio -NER)) katika elimu ya msingi kutoka asilimia 94.0 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia100.
Changamoto zingine nipamoja na kuinua kiwango cha ufaulu katika ngazi zote za elimu, kuongeza nafasi za wanafunzi wanaojiunga na elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi, elimu sekondari ya juu na elimu ya juu.
Kuongeza idadi na kuimarisha rasilimali watu, katika ngazi zote za elimu, kuongeza na kukarabati miundo mbinu ili kukidhi ongezeko la uandikishaji katika ngazi zote za elimu, kuinua idadi ya wananchi wanaoshiriki katika “Mpango wa Uwiano Kati ya Elimu ya Watu Wazima na Jamii”.
Kuongeza vitendea kazi, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na mitambo katika ngazi mbalimbali za elimu, kuimarisha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili kuwafanya wanafunzi na walimu kuwepo shuleni muda wote, kuimarisha ufundishaji na ujifunzaji hususani katika masomo ya lugha, hisabati na sayansi, kuimarisha mafunzo kazini endelevu katika ngazi zote za elimu, kuimarisha ukaguzi, ufuatiliaji na tathimini katika ngazi zote za elimu na kuboresha mazingira ya kufanyia kazi ya Wakaguzi wa shule.
Changamoto zingine ni kuimarisha muundo wa uongozi katika kusimamia utoaji wa elimu bora nchini, kukabiliana na ongezeko kubwa la watu wazima na vijana wasiojua kusoma na kuandika, Kuongeza bajeti ya elimu ili kuweza kutekeleza mipango ya sekta ya elimu kikamilifu, kuimarisha mawasiliano na wadau katika sekta ya elimu na kuboresha upangaji wa vipaumbele vyenye tija katika sekta ya elimu.
Matarajio ya Wizara kwa Miaka 50 ijayo
Matarajio ya wizara hiyo ni pamoja na kuinua ubora wa elimu katika ngazi zote kwa kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kutosha vya kufundishia na kujifunzia pamoja na kutoa visaidizi, vifaa vya kujifunzia na kufundishia kwa watu wenye mahitaji maalum, kuimarisha ufundishaji kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kutoa mafunzo na kuongeza ajira na kupanga waalimu kulingana na mahitaji walimu.
Matarajio mengine ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu hasa wale wanaopangwa katika maeneo ambayo hayafikiki kwa urahisi, kupitia na kuboresha mitaala ili iende sambamba na mabadiliko na mahitaji ya nchi na kuimarisha ufundishaji na kujifunza hususan kwa masomo ya hisabati, sayansi na lugha.
Kuongezeka fursa za elimu na usawa kwa kuweka mazingira bora ya kufundishia na kujifunzia kwa kujenga na kukarabati miundo mbinu ya elimu kama maabara, madarasa, maktaba, vyumba vya mihadhara, vyoo na nyumba za walimu na kukamilisha mapitio ya sera ya elimu na mafunzo na mikakati ya utekelezaji wake.
Malengo mengine ni kusimamia ubora wa elimu kwa kuimarisha ukaguzi wa shule, ufuatiliaji na tathmini ya elimu katika ngazi zote za elimu, kuimarisha na kujenga uwezo wa uongozi katika mipango ya elimu na kuimarisha maendeleo ya michezo katika kazi zote za elimu.
Kuandaa mafunzo kwa walimu wa shule za msingi na sekondari hususani kwa masomo ya sayansi, hisabati na lugha, kuinua kiwango cha uandikishaji wa watoto wa rika lengwa wa elimu ya msingi kutoka asilimia 95.4 na kufikia asilimia 100 mwaka 2015, kufanya ukaguzi wa shule kuwa wakala wa serikali na kuanzishwa kwa ‘Teachers’ Professional Board’ ili kuinua ubora, umahiri na maadili ya ualimu.
Makala hii imetolewa kwenye gazeti la Raiamwema la tarehe 9 decemba 2011.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni