Wanafunzi hawa wako darasani wakijifunza ushonaji. Serikali inasema inachukua hatua kadhaa kuhakikisha wahitimu wanamaliza masomo wakiwa na uwezo wa kufanya vyema katika soko la ajira kwa kujiajiri, kuajriwa au kuajiri. Picha na Maktaba
Uzoefu na tafiti vinaonyesha vijana wanaohitimu katika ngazi mbalimbali za elimu nchini wanakabiliwa na changamoto ya kupata ajira.
Hata hivyo, hilo siyo tatizo la Tanzania pekee, bali ndivyo hali ilivyo karibu duniani kote. Ziko sababu nyingi zinazochangia hali hii kwa mujibu wa watafiti, ikiwamo mabadiliko ya haraka ya sayansi na teknolojia.
Nyingine ni athari za utandawazi na hata uduni wa mitalaa inayotumika shuleni na vyuoni, ambayo mwishowe hutoa wahitimu wasio na uwezo wa kupambana katika soko la dunia la ajira.
Elimu ya ujasiriamali
Huenda dawa ya tatizo hili kwa Tanzania ni kuhimiza utoaji wa elimu ya ujasirimali shuleni na vyuoni kama anavyobainisha Mkuu wa kitengo cha Ushauri na Unasihi katika Ofisi ya Kamishna wa Elimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Madina Kemilembe.
Anasema kwa hali ilivyo sasa nchini mitalaa haina budi kuwa na vipengele kuhusu ujasiriamali, elimu anayosema itawapa wahitimu uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa au kutoa ajira kwa wengine.
“Kwa tafsiri ya kawaida, ujasiriamali ni kuwaza na kutenda kijasiriamali kunakomfanya mtu kubuni, kuanzisha, kuboresha au kuhuisha thamani kwa mtu binafsi, kikundi, taasisi au jamii,” anatoa tafsiri ya ujasiriamali na kuongeza:
“Msingi wa ujasiriamali ni kutambua au kubuni fursa ikifuatiwa na uthubutu na kuchukua hatua katika kuitumia fursa hiyo.”
Kwa mujibu wa Kemilembe, tayari Serikali kupitia wizara imechukua hatua kadhaa kuhakikisha wahitimu wanamaliza masomo wakiwa na uwezo wa kufanya vyema katika soko la ajira kwa kujiajiri, kuajriwa au kuajiri.
Kwa mfano anasema mwaka 1997 wizara ilianzisha somo la Stadi za Kazi katika mtalaa wa elimu ya msingi, kwa lengo la kuwawezesha vijana kuwa na mtazamo chanya katika ulimwengu wa kazi, kujenga na kuendeleza vipaji vyao, kuwapa stadi za kazi na stadi za maisha.
“Mwaka 2002 Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ilitoa Waraka wa Elimu namba kumi na moja ukielekeza shule za msingi na sekondari kuanzisha huduma ya malezi na unasihi, ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi ya kitaaluma, kijamii na kisaikolojia kwa lengo la kukabiliana na changamoto za maisha yao ya kila siku kama vile mihemuko inayotokana na mabadiliko katika ukuaji wa kimwili, uhusiano na magonjwa mbalimbali ya kuambukiza kama vile Ukimwi,” anasema.
Huduma hiyo ya malezi anasema inajumuisha pia kuwapa wanafunzi miongozo na nasaha za kazi, kama vile kuchagua masomo, kuyaweza, kuyapenda na kutambua kazi anazoweza kufanya zinazoendana na masomo aliyoyachagua.
“Katika eneo hilo kuna kipengele cha elimu ya ujasiriamali na shughuli zake ambazo zimekuwa zikifanywa na wadau mbalimbali wa elimu lakini haziratibiwi,” anaongeza kusema.
Utafiti wa Shirika la Kazi Duniani
Mwaka 2001 Shirika la Kazi Duniani (ILO) kupitia programu iitwayo Ujasiriamali kwa vijana au ‘Youth Entrepreneurship Facility’, kwa kushirikiana na Taasisi ya Menejimenti na Maendeleo ya Ujasiriamali (IMED) walifanya utafiti wa kubaini juhudi za Tanzania katika utoaji wa elimu ya ujasiriamali.
Miongoni mwa malengo mahususi ya utafiti ilikuwa ni kutathmini na kujua ni kwa kiwango gani elimu ya ujasiriamali inafundishwa na umuhimu wake katika mazingira ya Tanzania, kutathmini mtalaa wa elimu uliopo kwa kuangalia malengo, matokeo, vifaa vya kufundishia na kujifunzia na njia zinazotumika kufundishia na kujifunzia katika kila ngazi.
Matokeo ya utafiti yalionyesha kuwa Sera ya Taifa ya mwaka 2004 inaitambua na kuipa uzito elimu ya ujasirimali katika mfumo wa elimu rasmi na usio rasmi.
Kutokana na hilo Baraza la Taifa la Uwezeshaji Kiuchumi liliandaa mwongozo kuhusu mkakati wa kitaifa wa elimu ya ujasiriamali unaotoa ujuzi wa ujasirimali ambao wanafunzi katika ngazi zote za elimu wanatakiwa waupate.
“Baada ya kupata matokeo ya tafiti kuhusu namna elimu ya ujasirimali ilivyo katika mfumo wa elimu, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa kushirikana na Shirika la Kazi Duniani, kwa kuanzia ilichagua mikoa minane ya majaribio,” anasema Kemilembe.
Anaongeza: “Katika kila mkoa ziliteuliwa wilaya mbili. Lengo likiwa ni kujua ni kwa namna gani walimu wa masomo chukuzi katika mikoa hiyo minane ya majaribio wanaweza kufundisha kwa ubora zaidi elimu ya ujasiriamali, ili ikionyesha mafanikio elimu hiyo itekelezwe katika mikoa yote.’’
Kwa mujibu wa Kemilembe Shughuli ambazo zimefanyika hadi sasa ni pamoja na kuundwa kwa kamati ya utendaji yenye wajumbe kutoka idara za Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Baraza la Uwezeshaji la Kiuchumi, Wizara ya Kazi na Maendeleo ya Vijana na Tamisemi.
Jukumu kubwa la kamati lilikuwa ni kusimamia utekelezaji wa programu ya elimu ya ujasiriamali kuanzia ngazi ya taifa, halmashauri na kuandaa mpangokazi.
Majukumu mengine ni kuendesha semina elekezi kwa wadau wa elimu kutoka mikoa minane ya majaribio na katika halmashauri zilizoteuliwa, kwa lengo la kuwahamasisha kuhusu elimu ya ujasiriamali.
Kuendesha mafunzo kwa walimu 128 wa masomo chukuzi wanaotoka katika mikoa na wilaya za majaribio ili waweze kufundisha kwa kutumia muhtasari uliochopekwa masuala ya ujasiriamali