Wanafunzi wakiwa katika Mahafali yao
Na Fredy Azzah, Mwananchi
Hivi karibuni Shirikisho la Wamiliki na Mameneja wa Shule na Vyuo visivyo vya Serikali (Tamongsco), liliutangazia umma kuanza kwa mfumo mpya wa kuandikisha wanafunzi wa kujiunga na kidato cha kwanza na cha tano kuanzia mwaka 2014.
Kwa mujibu wa taarifa kwa umma iliyotolewa hivi karibuni na Tamongsco, kupitia utaratibu huo waliouita shirikishi, kamati maalumu imeundwa kusimamia uandikishaji wa wanafunzi katika shule za umma na zile binafsi.
“Lengo ni kutambua kila mwanafunzi na udahili wake katika shule ili kuondoa uwezekano wa wanafunzi kuchaguliwa katika zaidi ya shule moja na kuzifanya baadhi ya shule kutokuwa na wanafunzi kwa sababu ya wanafunzi kupata udahili katika shule zaidi ya moja,” inasema taarifa hiyo na kuongeza:
“Utaratibu huu mpya wa udahili ni maalumu, kila mwanafunzi aliyedahiliwa atapatiwa namba maalum ambayo ndiyo atakayoitumia katika maisha yake yote ya elimu. Asipoingizwa katika utaratibu huu atapata matatizo huko aendako,” inasema taarifa hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati itashirikisha
viongozi wa mikoa, Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) na Tamongsco yenyewe.
Baadhi ya kazi za kamati zitakuwa ni kushiriki katika vikao vya udahili wa wanafunzi, kutekeleza miongozo na maelekezo ya udahili yatakayotolewa na Kamishna wa Elimu, huku viongozi wa mikoa na wakifuatilia orodha ya wanafunzi waliodahiliwa katika shule zilizo chini ya Tamongsco.
Mwananchi liliweza kuona barua kutoka kwa Kamishna wa Elimu kwenda kwa watekelezaji wa utaratibu huo ikieleza kwamba, baada ya Necta kutangaza matokeo ya darasa la saba, utaratibu unaoendelea sasa ni kila mkoa kuchagua wanafunzi watakaoendelea na kidato cha kwanza mwaka 2014.
“Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, imeandaa mfumo wa kielektroniki wa udahili wa watahiniwa watakaoendelea na masomo katika ngazi ya kidato cha kwanza,” inasema sehemu ya barua hiyo.
Tamongsco yasifu
Mwenyekiti wa Tamongsco , Mahmoud Mringo anasema kuwa, utaratibu huo ni hatua ya kwanza katika kuelekea ushirikishwaji wa sekta binafsi ambao wadau wake wamekuwa wakiuomba kwa muda mrefu sasa.
“Suala halitokuwa kufanya udahili pekee, Hivyo vikao vitakapokuwa vikifanyika vitasaidia kuangalia matatizo yanayokabili sekta ya elimu kwenye eneo husika na kutafuta njia za kuyakabili,’’anasema na kuongeza:
“ Kwa kuwa kutakuwa na wadau muhimu wa elimu wa mkoa mzima, wataangalia ubora wa ufaulu kwa mwaka husika, ufanisi wa walimu, ushiriki wa wazazi na mambo mengine ambayo kwa ujumla wake yatasaidia kuinua elimu yetu.”
Usajili kidato cha tano
Hata hivyo, Mringo anasema udahili wa pamoja hauwezi kuongeza wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano, kwani bado vigezo na sifa za kwenda kwenye ngazi ya juu ya elimu zitazingatiwa.
Anasema kwa kuwa moja ya malengo ya Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa ni kuongeza ufaulu kwa wanafunzi waliohitimu kidato cha nne mpaka kufikia asilimia 61, lazima Serikali ihakikishe wanafunzi wote watakaofaulu wanapata nafasi ya kuendelea na kidato cha tano.
“Wanafunzi waliofanya mtihani huo ni karibu 400,000 asilimia 60 ni kama watoto 300,000. Nusu yake ambao ni kama watoto 150,000 watakuwa na sifa za kuendelea na masomo kwa ngazi za juu.
‘’Shule za Serikali zinaweza kuchukua watoto 70,000, ili kuchukua wote watakaofaulu lazima Serikali iongeze shule zake zaidi ya mara mbili ya zilivyo leo. Suala hilo haliwezekani kwa hiyo kushirikisha shule binafsi ni muhimu zaidi, ingawa pia hata na wao hawawezi kuchukua watoto wote hao,” anasema.
Kutokana na hali hiyo anasema kuwa lazima Serikali iboreshe mfumo wa elimu wa mwanafunzi kuendelea na elimu katika vyuo vya kada ya kati na ufundi baada ya kuhitimu kidato cha nne.
Anasema kuwa, kufanya hivyo kutawapa fursa watoto wengi kujiendeleza kuliko kuwaaminisha wote kuwa lazima waende kitato cha tano
“Siku hizi kuna wanahitimu wengi wa kidato cha nne wenye sifa za kwenda kidato cha tano, lakini wanachagua kwenda kwenye hivi vyuo. Suala hili lazima liangaliwe kwa umakini na mfumo huu uboreshwe pia,” anasema Mringo.
Kwa upande wake, Profesa Ruth Meena anasema mfumo mpya wa udahili wa pamoja ni moja ya mambo ambayo wamiliki wa shule binafsi wamekuwa wakiyakipigia debe kwa muda mrefu.
“Tangu mwanzo tulikuwa tunataka hicho kitu, kukaa kwenye meza moja kuwachagua watoto kuna faida nyingi. Wenzetu kwenye nchi nyingine wameanza kitu hiki siku nyingi na wanashirikiana mambo mengi sana siyo kuchagua watoto tu,anaeleza.
Anaongeza: ‘’Ukiangalia kama Zimbabwe Serikali inaona kuwa shule binafsi ni washiriki na siyo kama sisi hapa shule binafsi zinaonekana kama washindani.”
Anasema kuwa, ushirikiano huo usiishie kwenye usajili wa wanafunzi tu, uende mbali ikiwa ni pamoja na kuzisaidia shule binafsi kama vile kuzipa vitabu na ruzuku.
“Kwa sasa hivi ukiangalia hata mtoto anayetoka shule za watu binafsi ni vigumu kupata mkopo anapofaulu kwenda chuo kikuu, kisa wanasema kasoma shule ya gharama, hii siyo hata hata kidogo,” anaeleza.
Anasema kuwa, kuwekeza kwenye sekta ya elimu siyo biashara hivyo ni vyema Serikali ichukulie watu wenye shule binafsi kama watoa huduma na washirikiane nao kama inavyofanya kwa wamiliki wa hospitali.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni