Jumanne, 7 Januari 2014

Zimepotea wapi hamasa za matokeo ya darasa la saba?


Kuna njia nyingi za mtu kujielimisha. Kwa mfano, wapo wanaopata maarifa baada ya kufanya makosa fulani.
Nijitolee mfano mimi mwenyewe. Kwa wanaokumbuka zamani kulikuwa na aina ya redio za betri maarufu kwa jina la ‘National.’
Nikiwa shule ya msingi, neno hilo nilizoea kulisoma kwa jina la ‘nationali’ Sikusoma ‘neshno au nashno kama linavyotamkika kwa wenyewe wenye lugha yao.
Siku niliyojua kulitamka kwa usahihi, ni pale nilipotamka kimakosa mbele ya mjuzi mmoja aliyeniambia; ‘’we umekosea’’ Tangu siku hiyo nilijifunza kutamka ‘neshno’ badala ya ‘nationali’
Mfano mwingine na ambao ndiyo ulionisukuma kuandika makala haya unahusu maneno mawili tuliyoyakopa kutoka katika Kiingereza. Nayo ni kupasi (pass) na kufeli (fail).
Kipindi hichohicho cha uanafunzi wa elimu ya msingi, niliyatumia maneno haya ndivyo sivyo.
Nilijua kupasi (kwa maana ya pass the exam) ndiyo kufeli na kufeli ni kufaulu au kupasi.
Ama kwa hili la kuchanganya tofauti kati ya kupasi na kufeli, sikujua ukweli wa maana ya maneno hayo mpaka nilipokaribia kuhitimu elimu ya msingi, hasa pale nilipoanza kufuatilia matokeo ya wanaomaliza darasa la saba.
Kwa wanaokumbuka kuanzia miaka ya 1990 na kurudi nyuma, matokeo ya darasa la saba yalikuwa ni tukio muhimu kwa Taifa.
Enzi hizo kuanzia wahitimu wenyewe, wazazi na wadau wengine wakiwamo wanafunzi wanaoendelea na masomo, kipindi cha kutangazwa matokeo kilikuwa na mvuto na hamasa ya aina yake.
Kipindi hiki kilipofika, kila mtu alijua. Na hata habari na mazungumzo katika kila kona mitaani ilikuwa ni kupasi au kufeli.
Mwaka fulani katika kipindi hiki, ndipo nilipokuja kubaini maana halisi ya maneno kupasi na kufeli. Hamasa za kutaka kujua nani anaingia sekondari nani alichemsha, ndizo zilizoniwezesha kujua kuwa kupasi ilimaanisha mtu kufaulu yaani kwenda sekondari na kufeli ni kushindwa kwa maana ya kukosa fursa ya kwenda sekondari za Serikali.
Enzi hizo shule za Serikali nchini kote zilikuwa na thamani isiyomithilika. Kila mwanafunzi alitamani kusoma shule za Serikali, ndiyo maana kipindi hicho kulikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wanaorudia darasa la saba hata kwa majina ya kughushi.
Je, hali ikoje sasa? Tarehe 27 Desemba mwaka jana, nilikuwa naangalia runinga nikimtazama Katibu Mkuu wa Tamisemi, Mwalimu Abdalah Sagini akitangaza matokeo ya darasa la saba.
Kwanza sikujua kuwa siku hiyo eti kungetolewa taarifa hiyo muhimu kwa wananchi. Pili hata kesho yake, licha ya kila chombo cha habari hasa magazeti kuandika habari hiyo kwa uzito mkubwa, hapakuwepo na hamasa yoyote kuhusu matokeo hayo.
Nani ahamasike au aumwe tumbo kujua kama mwanawe amefaulu ama la, wakati siku hizi wazazi, walezi na hata wanafunzi walishakosa imani na shule za umma?
Wako wanaofikia hatua ya kuwatoa watoto wao shule za Serikali na kuwahamishia shule binafsi.
Hamasa kwa shue zetu imepotea. Siyo siri kuwa shule zetu zina hali mbaya kitaaluma na ndio maana siku hizi hazifui dafu kwa shule binafsi.
Huu ni wakati wa sisi sote katika jamii kujiuliza, tunawezaje kuzinusuru shule zetu ili zirudi katika hadhi ya zamani ili ziwe kimbilio la kila mwanafunzi kama zamani

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni